Serikali kuu inawekeza katika mpango unaolenga kukuza uaminifu na pia kuhakikisha jamii mbalimbali zinaishi kwa amani katika kaunti ya Lamu na kote nchini.
Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki anasema serikali pia inakusudia kuboresha uhusiano kati ya jamii na maafisa wa usalama kama njia moja ya kuimarisha vita dhidi ya ugaidi.
Waziri Kindiki amewataja wazee, wanawake na viongozi wa vijana kuwa nguzo muhimu katika ukuzaji wa amani ya kudumu, mshikamano na ushindi dhidi ya magaidi hatari ambao wamehangaisha jamii katika kaunti ya Lamu kwa muda mrefu.
Aliyasema hayo katika eneo la Mkunumbi katika eneo bunge la Lamu Magharibi, kaunti ya Lamu alipofanya mkutano wa ushauriano na wazee na wawakilishi wa jamii mbalimbali za kaunti hiyo.
Maafisa waandamizi wa usalama wakiongozwa na kamishna wa kanda hiyo ambaye pia anaongoza Kamati ya Usalama na Ujasusi ya Kanda ya Pwani Rhoda Onyancha pia walikuwapo.