Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki amesema majukumu yake ni kumsaidia Rais William Ruto katika majukumu yake na wala sio kumkosoa wala kumpinga.
Kwenye mahojiano ya moja kwa moja kupitia runinga za humu nchini siku ya Alhamisi kutoka nyumbani kwake mtaani Karen, Prof. Kindiki amesema atajitolea katika utendakazi wake.
Kuhusu suala la kuwa na ushawishi eneo la Mlima Kenya, Naibu Rais huyo alijitenga kujihusisha na siasa na badala yake kuendeleza ajenda ya serikali.
Aidha, amesema hajutii jinsi alivyoteuliwa baada ya mtangulizi wake kutimuliwa kupitia kwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Kuhusu suala la serikali kupoteza umaarufu, Kindiki amesema ni uhuru wa kidemokrasia kwa eneo lolote nchini kuwa na mtazamo tofauti na kinzani na serikali.
Prof. Kindiki aliteuliwa kuwa Naibu Rais baada ya Bunge la Taifa na lile la Seneti kuidhinisha hoja ya kumbandua madarakani mtangulizi wake Rigathi Gachagua.
Haya ndio yaliyokuwa mahojiano ya kwanza yaliyorushwa moja kwa moja na vyombo vya habari kutoka nyumbani kwake mtaani Karen tangu alipotwaa wadhifa huo.