Kindiki: Maafisa wa usalama wamepiga hatua North Rift

Marion Bosire
2 Min Read
Waziri Kindiki kwenye mkutano wa usalama Samburu

Waziri wa mambo ya ndani Profesa Kithure Kindiki amesema kwamba maafisa wa usalama katika eneo la kaskazini la bonde la ufa, wamepiga hatua kubwa katika kukabiliana na ujambazi.

Kindiki alisema kwamba kwa muda wote wa miezi minane ambayo kikosi hicho cha “Operation Maliza Uhalifu” kimekuwa katika eneo hilo, serikali imekuwa ikitekeleza uangalizi wa mara kwa mara.

Alisema lengo la uangalizi huo ni kufahamu mafanikio yaliyopatikana na changamoto ili kushughulikia mianya yoyote iliyopo.

Lengo kuu kulingana naye ni kumaliza kabisa ugaidi wa wezi wa mifugo waliojihami ambaso wamesababisha vifo na hasara dhidi ya wakenya wasiokuwa na hatia kwa muda wa miaka mingi sasa.

Kulingana naye ujambazi katika kaunti ya Samburu umedhibitiwa huku mafanikio makubwa yakiafikiwa katika eneo la Baragoi ambalo hushambuliwa sana.

Hivi leo, waziri Kindiki alifanya mkutano wa kujifahamisha na kuongeza nguvu oparesheni hiyo katika afisi ya chifu wa lokesheni ya Kisima, Divisheni ya Suguta Marmar, eneo bunge la Samburu Magharibi.

Alikutana na wanachama wa kamati ya usalama na ujasusi ya eneo la Rift Valley, wenzao wa kaunti ya Samburu na makamanda wa oparesheni hiyo katika eneo hilo.

Kindiki alisema serikali imejitolea kuhakikisha oparesheni ya Maliza Uhalifu inaendelea vyema ili kutokomeza kabisa ujambazi na wizi wa mifugo kaskazini mwa Kenya.

Alisema maafisa wa usalama wameelekezwa kukabiliana na wawezeshaji wote wa ujambazi iwe ni wanasiasa, wanabiashara au viongozi wa dini pamoja na wanaopanga mashambulizi.

Website |  + posts
Share This Article