Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki ametetea mfumo wa usimamizi wa serikali kuu akisema unaweza kutumiwa kuunganisha ajenda ya serikali ya kitaifa mashinani.
Aliyasema hayo kwenye mkutano wa maafisa wakuu wa usimamizi wa serikali kuu uliohudhuriwa na Rais William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua katika taasisi ya mafunzo ya serikali huko Lower Kabete.
Mkutano huo uliwaleta pamoja makamishna wa maeneo, makamishna wa kaunti na manaibu kamishna wa maeneo mbali mbali.
Kindiki alisisitiza kwamba wakielekezwa ipasavyo, maafisa wa usimamizi wa serikali kuu wanaweza kutekeleza hilo kwani wanaelewa vyema sehemu mbali mbali za nchi.
Kulingana naye hatua ya Rais Ruto ya kuzungumza na maafisa hao leo itawamotisha kutekeleza kazi ya serikali kuu mashinani ipasavyo na kuhakikisha usalama na mshikamano vinadumu.
Huku akigusia mabadiliko yaliyopendekezwa na katiba kwenye mfumo huo wa maafisa wa serikali kuu nyanjani, Kindiki alisema sehemu kubwa ya mabadiliko hayo tayari yametekelezwa na kwamba mianya michache iliyosalia itazibwa.
“Mengi kati ya mabadiliko yanayohitajika yametekelezwa lakini kuna machache ya kisera na kimfumo yamesalia ambayo yatatekelezwa ili kuhakikisha mshikamano zaidi na kuwa wa maana kwa serikali ya Kenya ambayo ndiyo mwajiri wetu.” alisema Kindiki.