Mgomo wa Madaktari uliopangwa kuanza Jumapili ijayo, usiku wa manane, na kulemaza huduma katika hospitali zote za umma umefutiliwa mbali.
Hii ni baada ya viongozi wa Chama cha Madaktari, KMPDU, jana jioni kuafikiana na serikali kuhusu masuala tata wakati wa mkutano uliohudhuriwa na Naibu Rais Kithure Kindiki na Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa miongoni mwa maafisa wengine wakuu serikalini.
Madaktari hao waliafikiana baada ya mkutano ulioandaliwa nyumbani kwa Naibu Rais mtaani Karen.
Kindiki aliahidi kuwa Madaktari hao watalipwa kiwango cha pesa walizoafikiana na serikali hivi karibuni katika akaunti zao za benki.
Kulingana na mwafaka huo, Madaktari wanagenzi watapokea shilingi 206,000 kwa mwezi kuanzia mwezi huu.
Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah, alifichua kuwa pia Madaktari watapokea malimbikizi ya asilimia 50 ya mishahara yao haraka iwezekanavyo.