Kindiki akanusha madai ya utoaji hongo katika makazi yake ya Karen

Amesema mikutano hiyo inalenga kujadili masuala ya maendeleo.

Marion Bosire and Lydia Mwangi
2 Min Read

Naibu Rais Kithure Kindiki leo amekanusha madai kwamba mikutano ya mashauriano anayofanya katika makazi yake ya Karen inatumika kuhonga watu.

Amesema mikutano hiyo, ambayo hukutanisha makundi kutoka kaunti mbali mbali katika makazi yake rasmi, inalenga kujadili masuala ya maendeleo.

Alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kuwezesha wananchi uliofanyika katika Wadi ya Githioro, eneo bunge la Kipipiri.

Kindiki alialika ujumbe kutoka kaunti ya Nyandarua katika makazi yake ya Karen wiki ijayo ili kujadili miradi ya maendeleo katika kaunti hiyo, baadhi ikiwa imesimama.

Mkutano huo pia utajadili utoaji wa hatimiliki kwa wamiliki wa ploti katika vijiji vya kikoloni. Aliongeza kuwa serikali imepata fedha za ujenzi wa barabara ya lami ya Geta-Ndunyu Njeru, ambayo awali ilikuwa imekwama.

Kindiki aliwashauri watu wa Mlima Kenya kutoingizwa katika siasa za mgawanyiko.

Kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wa alisema yeye ni miongoni mwa viongozi wengi kutoka eneo la Mlima Kenya walio kwenye serikali ya Rais William Ruto.

Alisisitiza umuhimu wa nafasi yake serikalini, akibainisha kuwa mawaziri humshirikisha katika masuala mbalimbali ya maendeleo.

Tofauti na wiki iliyopita ambapo ni madiwani wawili pekee waliohudhuria ziara ya Kindiki kaunti hiyo, safari hii madiwani tisa walioteuliwa na chama cha UDA walihudhuria.

Naibu Rais alitoa mchango wa Shilingi milioni 1.5 na Shilingi milioni 2 kutoka kwa Rais. Ichung’wa na Gitau walichangia kila mmoja Shilingi 500,000.

Website |  + posts
Share This Article