Kimbunga cha kitropiki kwa jina Jasper kimesababisha mvua nyingi kuliko kawaida ambayo pia imesababisha mafuriko makubwa katika eneo la kaskazini mashariki nchini Australia.
Kufikia sasa, watu wengi wamehamishwa kutoka kwa makazi yao katika eneo hilo ikitizamiwa kwamba makazi zaidi ya elfu 14 hayana umeme kutokana na hali hiyo.
Watu wengi walilazimika kupanda kwenye paa za nyumba zao kukwepa maji ambayo yalikuwa yakiongezeka kwa kasi kabla ya kuokolewa.
Katika jimbo la Queensland pekee, watu zaidi ya 300 waliokolewa na ndege za kijeshi usiku. Ndege hizo zimetolewa ili kusaidia katika shughuli za uokozi katika eneo hilo ambalo barabara zake hazipitiki.
Eneo linalopendwa sana na watalii la Cairns, halifikiki kabisa kwa sababu ya mafuriko na kuna hofu kwamba wakazi wapatao elfu 160,000 wa mji huo wataishiwa maji safi ya kunywa hivi karibuni.
Mji huo ulipokea milimita 600 za mvua kulingana na wataalamu katika muda wa saa 40, kiwango ambacho ni mara tatu ya kiwango cha kawaida kila mwezi wa Disemba.
Safari za ndege zimesimemamishwa kabisa kutoka na kuingia katika uwanja wa ndege wa Cairns ambapo ndege zinasemekana kuzingirwa na maji ya mafuriko.