Halfa iliyoandaliwa na ubalozi wa Eritrea jijini Tel Aviv nchini Israel ya kuadhimisha miaka 30 ya uhuru wa Eritrea ndiyo ilichochea mapigano kati ya makundi mawili hasimu ya raia wa Eritrea waliokimbilia Israel.
Wanaounga mkono serikali ya rais Isaias Afwerki ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 30 walikuwa wamekusanyika kwenye ubalozi huo kwa sherehe hizo huku wanaopinga uongozi wake wakiandamana hadi eneo la sherehe na kuivuruga.
Rais Isaias Afwerki amekuwa akiongoza Eritrea tangu ilipojipatia uhuru kutoka kwa Ethiopia na hajawahi kuandaa uchaguzi, kuunda bunge au idara huru ya mahakama.
Amepiga marufuku vyama vya kisiasa huku akiorodheshwa kuwa miongoni mwa viongozi wabaya zaidi ulimwenguni hasa katika uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.
Wanaopinga serikali yake na ambao wametorokea Israel walihisi kwamba sherehe hizo zilikuwa za kusherehekea uongozi wa kiimla, ikitizamiwa kwamba wamekwepa nchi yao kutokana na hali duni.
Walikuwa wengi kiasi kwamba walizidi maafisa wa polisi waliokuwepo, wakaingia katika eneo hilo ambapo walipasua viti na madirisha hatua iliyochochea wanaounga mkono serikali ya Afwerki kuanza kupigana nao.