Kikosi cha Afrika Mashariki chatakiwa kuondoka DRC

Tom Mathinji
1 Min Read
DRC yataka kuondolewa kwa kikosi cha Afrika Mashariki.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imesema kikosi cha kulinda amani cha mataifa ya Afrika Mashariki kimeshindwa kukomesha ghasia nchini humo na lazima  kiondoke ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

“Wameshindwa kutatua tatizo lililopo,” alisema msemaji wa serikali Patrick Muyaya.

Kwa mujibu wa Muyaya,  waasi wa kundi la M23 wamekataa kuondoka katika maeneo waliyotwaa kuambatana na makubaliano ya mkataba uliotiwa saini nchini Angola mwaka uliopita.

Muyaya alisema viongozi wa serikali katika kanda ya Afrika Mashariki wanafaa kukutana na kutoa uamuzi kuhusu kushindwa kwa kikosi hicho kutatua mzozo unaoendelea nchini humo.

“Mkutano wa viongozi hao unapaswa kutangaza kushindwa kwa kikosi cha kulinda amani kukabiliana na tatizo hilo,” aliongeza Muyaya.

Tangu mwezi Novemba mwaka jana, wanajeshi kutoka Uganda, Burundi, Sudan Kusini na Kenya wamekuwa DRC katika juhudi za kurejesha amani katika eneo la Kivu Kaskazini linalokumbwa na ghasia.

Eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini limekumbwa na ghasia kwa muda wa miongo miwili, huku makundi tofauti yaliyojihami yakiendeleza mashambulizi licha ya kuwepo kwa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1999.

TAGGED:
Share This Article