Kikao cha tatu cha tume ya pamoja ya ushirikiano kati Kenya na Somalia kiliandaliwa leo ambapo ujumbe wa Kenya uliongozwa na naibu Rais Rigathi Gachagua.
Naibu Rais alisema kwamba Kenya inajizatiti kuboresha uhusiano kati yake na nchi nyingine kama mojawapo ya mikakati ya kujenga uchumi dhabiti.
Alisema hatua ya taifa la Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC inapanua fursa za ushirikiano katika biashara na viwanda, kilimo, uchumi wa baharini, teknolojia na sekta nyingine.
Kikao hicho kilifanyika katika makazi rasmi ya naibu rais mtaani Karen, Nairobi na ujumbe wa Somalia uliongozwa na waziri mkuu Hamza Abdi Barre.
“Tunaporekebisha miundomsingi na kupanga mifumo ya ujenzi kupiga jeki maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ajili ya watu wa mataifa haya mawili, tuko mahali pazuri ambapo tunashirikiana kwa amani na usalama katika kanda.” alisema Gachagua.
Alitoa shukrani kwa waziri mkuu wa Somalia na ujumbe wake kwa mkutano huo kwa niaba ya serikali ya Keya inayoongozwa na Rais William Ruto.