Kikao cha Maseneta wote kwa sasa kinaendelea katika Bunge la Seneti kwa lengo la kusikiza mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Mawakili wa pande zote, wakiwemo mawakili wa Naibu Rais na wale wa Bunge la Taifa tayari wamefika Seneti kushiriki kikao hicho.
Aidha, Gachagua tayari amewasili katika Bunge la Seneti ili kujibu mashtaka dhidi yake.
Kikao hicho kitaandaliwa leo Jumatano na kesho Alhamisi na kisha Maseneta kupiga kura kuunga au kupinga hoja hiyo baada ya kupima kwa mizani ushahidi uliowasilishwa.
Kikao hicho kinaandaliwa baada ya Mahakama Kuu kukataa kuzuia Seneti kusikiza mashtaka dhidi ya Gachagua.
Gachagua anakabiliwa na mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi yake kupitia hoja maalum ya mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Mutuse ni miongoni mwa mashuhuda wa Bunge la Taifa watakaowasilisha ushahidi dhidi ya Gachagua wakati wa kikao hicho.
Hoja ya kutaka Gachagua afurushwe kwenye wadhifa huo tayari imepitishwa na Bunge la Taifa na ikiwa itapitishwa katika Seneti, basi Gachagua atapoteza wadhifa huo.
Maseneta 45 kati ya 67 wanahitajika ili hoja hiyo kupita katika Seneti.
Ikiwa Maseneta 23 watapinga hoja hiyo, basi Gachagua atakuwa amenusurika na ataendelea kuhudumu kama Naibu Rais.