Kijana kutoka Oljororok akataa kukata tamaa, atengeneza ‘gari’

Tom Mathinji
3 Min Read
Anthony Karumba Muriithi, atenegeneza gari licha ya kuwa hana elimu ya juu.

Baada ya kukamilisha mtihani wa kidato cha nne wa KCSE wa mwaka 2021, matumaini ya Anthony Karumba Muriithi ya kuendeleza masomo yake yaligonga mwamba.

Bongo yake ilisheheni mawazo ya uvumbuzi chungu nzima. Lakini jinamizi la ufukara lililoiandama familia yake lilikuwa kikwazo tosha cha kukwamisha ndoto yake. Lilidhihirisha ukweli wa msemo kwamba dau la mnyonge haliendi joshi.

Huku lengo lake la kuendelea na masomo likizidi kudidimia, Karumba aliazimia kutafuta kazi zisizo rasmi katika kijiji chake cha Mbombo, eneo bunge la Ol Jororok, kaunti ya Nyandarua. Lengo lilikuwa kukimu mahitaji yake ya kila siku.

Hata hivyo, azima ya Karumba ya kutengeneza gari ilimwandama kila uchao. Uzito wa azima hiyo ulipomuelemea,  alikata shauri ya kulivalia njuga swala hilo.

Ndoto hiyo ya mtanashati huyo mwenye umri wa miaka 20 ya kutengeneza gari, ilianza pale alipoanza kununua vyuma vikuu kuu, alivyovitumia kutengeneza baiskeli yake ya kwanza mwaka 2019.

Kutokana na changamoto si haba alizokabiliana nazo, Karumba wakati mmoja alivunjika moyo na hata alihisi kupiga kumbo shughuli hiyo, lakini alijizatiti na kutengeneza kifaa cha kufyeka nyasi ambacho hadi sasa kinatumiwa.

Karumba aliyesomea shule ya upili ya wavulana ya Leshau, anasema upendo aliokuwa nao kwa mashine tangu utoto wake ulimnata kama kupe. Wala haukuwezesha mawazo yake kupiga hata hatua moja na kuhamia tasnia nyingine, licha ya changamoto sufufu zilizomwandama.

Aliamua kuzizibia masikio changamoto mzo zilizomzingira kulia na kushoto na hatua baada ya nyingine, aliamua kusonga mbele aste aste. Muda si muda, alikumbatia utengenezaji gari.

Barubaru huyo alikuwa tayari amepata malighafi, ikiwa ni pamoja na zile alizotumia kutengeneza baiskeli. Sasa alipiga moyo konde na kuogelea katika bahari ya sekta ya utengenezaji bidhaa.

Licha ya kuwa Karumba hakuwahi jiunga na chuo chochote cha kiufundi, alitia bidii ya mchwa katika azima yake hiyo na hatimaye alitenegeneza gari ambalo familia yake hutumia kwenda kanisani.

Ndoto yake kuu ni kuwa mhandisi wa utenegenezaji magari. Karumba sasa anatoa wito kwa wahisani kumpiga jeki ili apate elimu na ujuzi ufaao.

Wito wake uliungwa mkono na wazazi wake James Muriithi na Ruth Wanja. Wawili hao wanasema walimsaidia mwanao kadiri ya uwezo wao, hadi pale babake Karumba alipougua na kulemewa kumsomesha kijana huyo aliyepata alama ya C+ katika mtihani wa KCSE.

Ombi la majirani wao pia ni kuona Karumba akitimiza ndoto yake na kufanikiwa maishani.

Share This Article