KEWOPA kuandaa hafla ya kuzindua maadhimisho ya uanaharakati dhidi ya dhuluma za kijinsia

radiotaifa
2 Min Read
Leah Sankaire, mwenyekiti KEWOPA

Leo, Novemba 25, 2024 ni siku ya kimataifa ya juhudi za kutokomeza dhuluma za kijinsia hasa dhidi ya wanawake.

Siku hii ni mwanzo pia wa maadhimisho ya siku 16 za uanaharakati dhidi ya dhuluma za kijinsia na muungano wa wabunge wa kike nchini KEWOPA unatarajiwa kuandaa hafla ya kuzindua maadhimisho ya mwaka huu.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya muungano huo na viongozi wengine wa kike nchini kukutana na Rais William Ruto kujadiliana kuhusu ongezeko la mauaji ya wanawake nchini.

Katika mkutano huo, iliafikiwa kwamba kampeni ya “Safe Homes, Safe Spaces” yaani nyumba salama, maeneo salama, iendeshwe na viongozi hao katika kipindi cha maadhimisho hayo.

Kiongozi wa nchi alitengea kampeni hiyo shilingi milioni 100 na inaaminika kwamba ndiyo viongozi hao wanazindua leo.

Novemba 25 ilichaguliwa na wanaharakati wa haki za wanawake kuwa siku ya kimataifa ya juhudi za kutokomeza dhuluma za kijinsia hasa dhidi ya wanawake, kwa sababu siku hiyo mwaka 1960 kina dada watatu maarufu kama “Mirabal sisters” waliuawa.

Mauaji yao yalitekelezwa kufuatia amri iliyotolewa na kiongozi wa kiimla wa wakati huo wa Dominican Republic Rafael Trujillo.

Dada hao walikuwa wanne Adela, Patria, Minerva na María Teresa na walikuwa watoto wa Enrique Mirabal Fernández waliokuwa kinyume na utawala wa Trujillo.

Hata hivyo Adela hakuhusika kwenye harakati za kupinga utawala huo wa kiimla lakini alikubaliana na harakati zao. Alifariki Februari Mosi, 2014 kutokana na sababu asili.

Mauaji ya dada zake watatu yalibadilika na kuwa ishara ya upinzani wa wanaharakati wa kike.

Share This Article