Kesi ya kusikiza kubanduliwa kwa Gachagua kurejelewa Jumanne

Martin Mwanje
1 Min Read

Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu litaanza tena kusikiza kesi ya kubanduliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Jumanne asubuhi.

Hii ni baada ya Mahakama ya Rufaa jana Jumatatu kukosa kutoa maagizo ya kuzuia jopo hilo kusikiza kesi hiyo.

Gachagua alikata rufaa jana Jumatatu akitaka jopo hilo kuzuiwa kuendelea kusikiza kesi hiyo.

Kulingana naye, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alikosea katika kuliteua jopo hilo kusikiza kesi ya kubanduliwa kwake kwani hana mamlaka hayo.  Gachagua anasema mamlaka ya kuteua majaji wa kusikiza kesi mahakamani yametengewa Jaji Mkuu.

Jopo la majaji hao watatu ambao ni Eric Ogola, Athony Mrima na Dkt. Freda Mugambi katika uamuzi wake lilisema Naibu Jaji Mkuu ana mamlaka ya kuwateua majaji kwa mujibu wa katiba, uamuzi ambao Gachagua ameupinga.

Majaji hao hususan wanatarajiwa kusikiza maombi ya kutaka maagizo ya kuzuia hatua ya Bunge la Seneti kumbandua Gachagua madarakani kuondolewa na mahakama.

Ikiwa mahakama itaondoa maagizo hayo, basi hatua hiyo itapisha kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki.

Hatua ya Gachagua kuwataka majaji hao kujiondoa kwenye kesi hiyo ilishindikana baada ya majaji kusema kuwa hakuna sababu za msingi zilizotolewa za kuwataka kufanya hivyo.

Share This Article