Kesi inayopinga utekelezwaji wa sheria ya fedha ya mwaka 2023 imeanza kusikizwa mapema leo Jumatano katika mahakama kuu ya Kenya.
Keshi hiyo inasikilizwa na majaji watatu ambao ni David Majanja, Christine Meoli na Lawrence Mugambi.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa leo na kesho Alhamisi kabla ya majaji kutafakari yaliyowasilishwa na kutoa uamuzi.
Walalamikaji katika kesi hiyo wanapinga uhalali wa sheria hiyo wakiitaja kuwa kinyume cha katiba na kuwa ilipitishwa bila kujumuisha maoni ya umma.
Kamati ya bunge kuhusu fedha nayo inatuhumiwa kwa kuchukua maoni kadhaa kutoka kwa wananchi na kuifanyia sheria hiyo marekebisho kabla ya kuidhinishwa na bunge.
Upande wa mashatka pia unadai kamati ya bunge haikuwa na mamlaka ya kupokea maoni ya wananchi na kufanyia marekebisho mswada kabla ya kuuwasilisha bungeni.
Jumla ya kesi tatu zinazopinga sheria hiyo ya fedha zinasikizwa na jopo hilo la majaji watatu ikiwemo kesi ya chama cha mawakili nchini, LSK na kesi ya senata wa Busia Okiya Omtatah.
Sheria ya fedha ya mwaka 2023 inajumuisha kuongezwa kwa matozo kadhaa na kuanzishwa kwa ushuru mpya na ilianza kutekelezwa mwezi Agosti.