Kenya yathibitisha kisa cha tatu cha Mpox

Tom Mathinji
1 Min Read

Wizara ya afya imethitisha kugunduliwa kwa kisa cha tatu cha ugonjwa wa Mpox jijini Nairobi.

Kupitia taarifa, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa afya Dkt. Patrick Amoth, amesema mwathiriwa huyo ambaye ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30, alikuwa na historia ya kusafiri nchini Uganda.

Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa mwathiriwa huyo ametengwa, akipokea matibabu.

Aidha, kulingana na Dkt. Amoth,  mgonjwa huyo yuko katika hali nzuri ya afya na  amekuwa akifuatiliwa kwa karibu katika eneo alimotengwa jijini Nairobi.

Kisa hiki cha hivi punde kinafikisha idadi ya visa vilivyothibitishwa vya ugonjwa wa Mpox hapa nchini, kuwa vitatu baada ya visa vingine viwili kugunduliwa awali.

Amoth amesema kwa jumla, sampuli 89 zimewasilishwa kwa uchunguzi ambapo sampuli 79 hazikupatikana na maambukizi, akiongeza kwamba sampuli saba zinaendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Kisa cha kwanza cha Mpox kiligunduliwa hapa nchini katika kaunti ya Taita Taveta, huku cha pili kikithibitishwa katika kaunti ya Busia.

Visa hivyo vitatu, vimehusishwa na waathiriwa hao kusafiri katika nchi za kigeni.

Share This Article