Kenya yashutumu mapinduzi nchini Niger

Martin Mwanje
1 Min Read

Kenya imelaani vikali mapinduzi nchini Niger ikayataja kuwa pigo kubwa kwa utawala wa demokrasia barani Afrika.

Rais William Ruto ametoa wito kwa pande husika kujizuia ili kutohatarisha maisha ya watu wa taifa hilo la Afrika Magharibi.

“Jamhuri ya Kenya inaungana na dunia katika kulaani vikali kitendo hiki kisichokuwa cha kikatiba kinachopindua demokrasia kupitia mapinduzi na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa Rais Mohamed Bazoum ambaye ameripotiwa kukamatwa na wanachama wa walinzi wa rais,” alisema Rais Ruto katika taarifa leo Ijumaa.

“Kenya iko tayari kusaidia kutatua mgogoro nchini Niger chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa ikiwa patakuwa na haja.”

Mapinduzi ya Niger ni ya saba Magharibi na Katikati mwa Afrika tangu mwaka wa 2020 na huenda yakawa na athari kubwa kwa mfumo wa demokrasia barani humo.

Mapinduzi hayo yalianzishwa na walinzi wa rais wanaotoka katika vikosi vya jeshi na kwa kawaida humlinda rais na ujumbe wake.

Viongozi wa dunia wamelaani mapinduzi hayo na kutoa wito wa mfumo wa kikatiba kurejelewa.

Website |  + posts
Share This Article