Timu ya taifa ya raga ya Kenya kwa wachezaji saba upande imeambulia nafasi ya 10, katika msururu wa tano uliokamilika mapema leo huko Hong Kong.
Shujaa ililemewa pointo 17-19 na Afrika Kusini, katika mchuano wa kuwania nafasi ya 9 na 10 na kujizolea pointi 3.
Ilikuwa mara ya tatu msimu huu kwa Kenya kumaliza katika nafasi ya kumi, baada ya kuafikia matokeo sawia katika misururu ya Dubai na Australia.
Kenya ingali katika hatari ya kushushwa ngazi ikisalia ya tisa kwa alama 18 kati ya mataifa 12 yanayoshiriki.
Argentina walidhihirisha ubabe wao baada ya kuibuka mabingwa wa kombe kuu kwa mara ya tatu msimu huu, wakiicharaza Ufaransa pointi 12-7 kwenye fainali.