Kenya yapigwa jeki kwa ruzuku ya shilingi bilioni 1 kukabiliana na kisukari

Dismas Otuke
1 Min Read

Kenya imepigwa jeki katika jitahada za kukabiliana na ugonjwa wa kisukari, baada ya kupokea ruzuku ya shilingi bilioni 1 kutoka wakfu wa kimataifa wa Kisukari, WDF.

Hela hizo zinatarajiwa kutumika kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Kenya ina jumla ya wagonjwa bilioni 2.1, wanaogua Kisukari lakini ni asilimia 40 pekee wanaopokea matibabu kutokana na gharama ya juu.

Hatua hiyo inajiri siku chache baada ya Waziri wa Afya Susan Nakhumicha, kuliongoza taifa kuadhimisha siku ya ugonjwa wa kisukari duniani Novemba 14, 2023.

Mandhari ya mwaka huu yalikuwa kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kisukari.

Nakhumicha alisema wizara yake iko makini kuhakikisha kwamba wagonjwa wa kisukari wanapata huduma hitajika.

Kulingana naye, wapo watu wengi wanaougua ugonjwa wa kisukari lakini hawafahamu huku wengine wakiendelea na matibabu.

Alishauri Wakenya wajiepushe na matumizi ya bidhaa za tumbaku na pombe.

Siku ya ugonjwa wa Kisukari duniani ilianzishwa mnamo mwaka 1991 na chama cha kimataifa cha kisukari kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani, WHO kama njia ya kuimarisha uhamasisho kufuatia ongezeko la wagonjwa wa kisukari duniani.

Website |  + posts
Share This Article