Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (NEMA), imetangaza mabadiliko makubwa katika uzoaji wa taka za carbon nchini, kama njia moja ya kuimarisha utunzaji mazingra.
Kulingana na mpangilio huo mpya taka zitakusanywa kwa mifuko isiyo ya plastiki inayoweza kuharibika baada ya matumizi.
Mwaka wa 2017, Serikali ya Kenya,ilipiga marufuku utengenezaji, uingizaji na matumizi ya mifuko midogo ya plastiki ya kubeba bidhaa kama njia ya kuzuia ueneaji wa plastiki katika mazingira.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Usimamizi wa Taka endelevu, 2022, NEMA imeamuru kwamba mashirika yote ya sekta ya umma na ya kibinafsi lazima yatenganishe taka zisizo hatari katika sehemu za kikaboni na zisizo za kikaboni, ziweke katika vipokezi vilivyo na lebo na rangi na kuhakikisha kuwa watoa huduma za taka wanakusanya na kushughulikia taka zilizotengwa ipasavyo.
Ili kutekeleza agizo hili, NEMA imetoa maagizo ambayo yataanza kutumika ndani ya siku 90 kuanzia tarehe ya notisi.
1. Taka zote za kikaboni zinazozalishwa nyumbani, taasisi za sekta ya kibinafsi na ya umma, taasisi za kidini na katika hafla lazima zitenganishwe na kuwekwa kwenye mifuko ya taka zinazoweza kuharibika kwa 100%.
2. Taka hizi za kikaboni zilizotengwa lazima zikusanywe kando na kusafirishwa hadi kwenye vifaa vilivyoteuliwa vya Urejeshaji nyenzo kwa usindikaji zaidi.
3. Matumizi ya mifuko ya plastiki kwa ajili ya kukusanya takataka sasa ni marufuku.
4. Serikali zote za Kaunti na watoa huduma za taka za kibinafsi walioidhinishwa na NEMA wanatakiwa kuwapa wateja wao mifuko ya kuzoa taka inayoweza kuharibika kwa asilimia 100 pekee.
Mpango huu unalenga kuhakikisha usimamizi mzuri wa mazingira wa taka za kikaboni, kupunguza utegemezi wa mifuko ya plastiki ya kawaida na kukuza matumizi ya njia mbadala endelevu.