Timu ya taifa ya raga ya Kenya kwa wanaume saba, upande almaarufu Shujaa, inakaribia kurejea kwenye mashindano ya msururu duniani baada ya kutwaa tena medali ya shaba katika mkondo wa pili wa ligi ya daraja ya pili mapema leo nchini Uruguay.
Shujaa imemaliza ya tatu katika msururu huo baada ya kuwashinda wenyeji Uruguay alama 22-14, katika mchuano wa mwisho.
Kenya ilizoa alama 16 kutoka kwa mkondo huo, ikiwa ya tatu kwenye msimamo kwa jumla ya alama 32.
Msururu wa tatu na mwisho utaandaliwa kati ya tarehe 28 na 29 mwezi huu mjini Sao Paulo, Brazil, huku timu nne bora zikipandishwa ngazi kushiriki msururu wa dunia mwaka ujao.