Kenya yamuunga mkono Jaji Njoki Ndung’u kuhudumu ICC

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi anasema Kenya inamuunga mkono kikamilifu Jaji Ndung’u kuwania wadhifa wa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Tom Mathinji
1 Min Read
Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Lady Justice Njoki Ndung’u.

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amesema serikali ya Kenya inamuunga mkono kikamilifu Jaji Njoki Ndung’u wa Mahakama ya Juu kuwania wadhifa wa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Akizungumza siku ya Alhamisi baada ya kushiriki mazungumzo na Jaji Mkuu Martha Koome na jaji Njoki Ndung’u afisini mwake, Mudavadi alidokeza kuwa maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Idara ya Mahakama, tayari wameanza kubuni mikakati ya kumpigia debe Jaji Ndung’u katika ngazi za kimataifa.

“Nimehakikishia Idara ya Mahakama kwamba mwaniaji wa Kenya katika mahakama ya ICC anaungwa mkono na kiongozi wa taifa Rais William Ruto na Baraza la Mawaziri,” alisema Mudavadi.

Baraza la mataifa wanachama wa ICC  linatarajiwa kuwachagua majaji sita wakati wa kikao chake cha 25 kitachoandaliwa jijini  New York nchini Marekani kuanzia Disemba 7-17 mwaka huu.

Kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, wawaniaji 15 walikuwa wameonyesha nia ya kuwania nyadhifa hizo huku wanane kati yao wakitoka bara Afrika.

Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje alisema wizara yake itatia bidii kumpigia debe Jaji Ndung’u kama aliyebora kwa wadhifa huo kutoka Kenya.

Share This Article