Kenya yamaliza ya pili baada ya kubanwa na Fiji Singapore 7’s

 Matokeo hayo yanaiacha Shujaa katika nafasi ya 9 msururuni kwa pointi 36 baada ya kumalizika kwa msimu.

Dismas Otuke
1 Min Read

Kenya imemaliza ya pili katika mkondo wa sita wa mashindano ya msururu wa dunia wa Singapore baada ya kushindwa na Fiji alama 12-21 katika fainali ya kombe kuu.

Nygel Amaitsa, alifunga try na conversion katika kipindi cha kwanza huku Shujaa wakiongoza alama 7-0 kufikia mapumzikoni.

Hata hivyo, Fiji walitumia tajiriba yao huku Viwa Naduvalo akifunga try mbili za haraka mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya Rauto Vakadranu, kuongeza try ya tatu.

Sakiusa Siqila, Filipe Sauturuga na Manueli Maisamoa walifunga conversion kwa Fiji huku William Mwanji akifunga try ya mwisho kwa Kenya kunako dakika ya 14.

Kenya imezoa pointi 18 kutokana na msururu huo, ingawa walikosa kusajili ushindi wa pili wa kombe kuu katika historia baada ya kuishinda Fiji mwaka 2016 na kutwaa kombe hilo.

Matokeo hayo yanaiacha Shujaa katika nafasi ya 9 msururuni kwa pointi 36, baada ya kumalizika kwa msimu.

Kenya inajiunga na Uruguay, Marekani na Ireland kushiriki mashindano ya mchujo yatakayoandaliwa Los Angeles kati ya tarehe 3 na 4 mwezi ujao, kuwania nafasi ya kufuzu kwa msururu wa msimu ujao.

 

Website |  + posts
Share This Article