Kenya imejiunga rasmi na Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo (IVI) kama nchi mwanachama.
Rais William Ruto amesema hatua ya Kenya kujiunga na taasisi hiyo inaimarisha azimio la kujitegemea katika uzalishaji wa chanjo.
Aliyasema hayo wakati wa hafla iliyofanyika kuadhimisha uidhinishaji wa mkataba wa Kenya kujiunga na IVI katika makao makuu ya taasisi hiyo mjini Seoul, South Korea leo Jumatano.
Wakati wa hafla hiyo, Ruto alipandisha bendera ya Kenya na kisha wimbo wa taifa kuchezwa.
Alisema ongezeko la upatikanaji wa chanjo utaboresha utoaji wa afya ya msingi humu nchini na kuunga mkono ipasavyo uzuiaji wa magonjwa.
Ruto alisema Kenya ilipata mafunzo muhimu kutokana na changamoto za kupata chanjo wakati wa janga la virusi vya korona, na kusisitiza dhamira ya kupunguza utegemeaji wa watengenezaji chanjo na bidhaa tiba zingine kutoka nje ya nchi.
“Wakati umewadia kwa Afrika kuhakikisha kuwepo kwa uhuru wa afya kwa kujikomboa kutoka kutegemea mipangokazi isiyokuwa endelevu, na kuharakisha mipango ya kujitegemea katika uzalishaji wa chanjo,” alisema Rais Ruto.
Aliongeza kuwa kufanya chanjo zipatikane kote duniani bila kujali utaifa na hadhi ni suala la dharura linalopaswa kuangaziwa.
“Katika masuala ya uzalishaji na usambazaji wa chanjo, hakuna yeyote aliye salama hadi kila mtu awe salama.”
Rais Ruto aliishukuru IVI kwa kutangaza kuwa itaanzisha afisi ya miradi jijini Nairobi akiongeza kuwa itaimarisha ajenda ya Kenya ya kuhakikisha upatikanaji wa afya kwa wote na kuhamasisha bara la Afrika kujitegemea katika uzalishaji wa chanjo.
“Chini ya suhirikiano huu, tutajizatiti kuimarisha mifumo yetu ya afya kwa kuhakikisha usalama wa bidhaa kupitia utafiti, uendelezaji na utengenezaji.”
Aliupongeza Umoja wa Afrika, AU kwa kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu ya afya, nguvukazi na mipango ya kitaasisi barani Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa IVI Jerome Kim alithibitisha kujitolea kwa taasisi hiyo kujenga mfumo imara na endelevu unaoendeleza sayansi, kuzuia magonjwa na kuokoa maisha.
“Wakati tukifikiria juu ya usalama wa chanjo, ni lazima uwe wa kimakusudi, unaowezesha na jumuishi,” alisema Kim.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alisema kuzuia magonjwa kupitia afya ya msingi ni nguzo muhimu ya mpango wa Kenya wa upatikanaji wa afya kwa wote.