Timu ya Kenya kwa wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20 imeanza vyema mashindano ya kuwania kombe CECAFA, baada ya kuwalaza wenyeji Tanzania mabao 2-1 katika uwanja wa KMC Jijini Daresalaam Jumapili alasiri katika pambano la ufunguzi kundini A.
Andrew Wangaya alipachika bao la kwanza dakika 23,kabla ya Andres Odhiambo kutanua uongozi kwa bao la pili dakika ya 66, huku Rahim Mkinyange alipachika la maliwazo kwa wenyeji dakika ya 76.
Kenya itarejea uwanjani Oktoba 10 kwa mchuano wa pili dhidi ya Rwanda na kumenyana na Eritrea tarehe 13 na kisha kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Sudan siku mbili baadaye.
Washindi wa kipute hicho watafuzu kwa fainali za AFCON za mwaka ujao.