Kenya, Uganda na Tanzania kuimarisha usalama Ziwa Victoria

Tom Mathinji
2 Min Read
Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo.

Serikali za Kenya,  Uganda, na  Tanzania, zimeshirikiana kushughulikia changamoto katika Ziwa Victoria ili kuimarisha usalama wa mpakani na ushirikiano baina ya nchi hizo tatu.

Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo,  alitangaza mipango kadhaa muhimu ambayo inaendelea, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa Kituo cha Operesheni cha Pamoja cha Bandari ya Kisumu, mafunzo ya pamoja ya baharini, na ununuzi wa magari ya doria ili kuimarisha shughuli za idara ya huduma za uhamiaji nchini.Omollo pia alipendekeza maswala  kadhaa

Dkt. Omollo aliyasema hayo wakati wa mkutano uliowaleta pamoja maafisa wa ngazi za juu kutoka Kenya, Uganda, na Tanzania, waliokutana kujadili mikakati ya kuimarisha usalama katika Ziwa Victoria na kutatua changamoto tata za uhalifu wa kimataifa katika kanda hii.

“Lengo la mkutano huu unaofadhiliwa na shirika la kimataifa kuhusu uhamiaji IOM, ni kutafuta mbinu za kushughulikia changamoto za kiusalama Ziwa Victoria,” alisema Omollo.

Katibu huyo pia alipendekeza  kuanzishwa Kituo cha uratibu wa uokoaji wa Baharini katika Ziwa Victoria, kuwianisha kanuni za uvuvi katika nchi zote tatu, kupanua programu za pamoja za mafunzo kwa maafisa walio katika mstari wa mbele, na kutangaza bandari nyingi za kuingia katika gazeti rasmi la serikali ili kufuatilia vyema maeneo maalum ya kuwasilisha samaki na maeneo mengine ya kuingilia.

Aidha, alidokeza kuwa Kenya imejitolea kupanua uchumi wake wa baharini, huku ikitambua uwezo wa ziwa hilo kuimarisha uchumi wa hapa nchini na Kanda hili kwa jumla.

Uganda iliwakilishwa na naibu kamishna wa uhamiaji na mkuu wa ujumbe wa Uganda Marcellino Bwesigye, huku Tanzania iliwakilishwa na mkuu wa utoaji mafunzo na ushirikiano wa Kimataifa  Ahmad Mwendadi.

Share This Article