Kenya, UAE kushirikiana kupanua mipango ya lishe shuleni

Martin Mwanje
2 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua (kulia) alipokutana na Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa UAE Mariam Almheiri

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo Jumatatu amesema Kenya inafanya kazi kwa lengo la kushirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE kupanua mipango ya lishe shuleni humu nchini kwa kusudi la kuongeza idadi ya watoto wananufaika na mipango hiyo. 

Gachagua aliyasema hayo alipokutana na Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi wa UAE Mariam Almheiri katika ofisi yake iliyopo Harambee House Annex.

Alisema nchi hizo mbili zina uhusiano mzuri na kwamba Kenya inatafuta kufanya kazi na UAE ili kupanua mipango ya lishe shuleni.

Almheiri anaongoza ujumbe wa UAE kuhudhuria Kongamano la Afrika kuhusu Tabia Nchi linalofanyika jijini Nairobi.

Mkutano kati yao unafuatia mwingine uliofanyika mjini Rome, Italia mwezi Julai walipokutana pembezoni mwa Mkutano wa 2 wa Mifumo ya Chakula wa Umoja wa Mataifa.

Wakati huo, Gachagua na Almheiri walikubaliana kutafuta njia bora za kupanua mipango inayoendelea ya utoaji lishe shuleni.

Leo Jumatatu, wawili hao walifanya mazungumzo yaliyohusiana na uwekaji wa hatua rafiki za mazingira katika kupanua mpango wa lishe shuleni nchini Kenya.

Gachagua alisema Kenya inafuata nyayo za nchi zingine kama UAE ambazo zimefanikiwa kuanzisha mipango ya utoaji lishe shuleni.

Alisema Kenya bado inadhamiria kuongeza idadi ya watoto wanaonufaika na mpango huo kutoka idadi ya sasa ya watoto milioni 1.8 hadi milioni 10 kufikia mwaka 2030.

Waziri wa UAE alisema nchi yake inatafuta njia ya kushirikiana na Kenya katika mipango ya utoaji lishe shuleni.

Aidha Waziri huyo aliipongeza Kenya kwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi akiitaja hatua hiyo kuwa nzuri kwa nchi zinazoendelea kuangazia changamoto zake na kupendekeza suluhu kwa mabadiliko ya tabia nchi.

Share This Article