Kampuni ya umeme ya Kenya Power, KP imeahidi kumaliza mrundiko wa maombi ya Wakenya ya kuwekewa stima katika muda wa siku 90 zijazo, wiki ya huduma kwa wateja inapoanza.
KP iko katika harakati za kutekeleza mpango wa majibu ya haraka katika kuwawekea wateja wapya mita kote nchini.
Akizungumza katika afisi za kampuni hiyo huko Stima Plaza kwenye hafla ya kuanzisha wiki ya huduma kwa wateja, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Mhandisi Joseph Siror alisema kwamba mpango huo wa majibu ya haraka utahakikisha maombi yote ya kuunganishiwa umeme yamekamilishwa ndani ya muda huo wa miezi mitatu.
“Katika siku zilizopita, tumeshuhudia changamoto katika manunuzi ya vifaa muhimu, hali ambayo imelemaza mpango wa kuongeza wateja wapya. Nina furaha kusema kwamba changamoto hizo zimeshughulikiwa na tumeanza kupokea mita ambazo tutagawa ili kuondoa mrundiko wa maombi ya kuunganishiwa stima,” alisema Siror.
Alisema pia kwamba kampuni hiyo ya umeme itaunganisha wateja wapatao 320,000 kwa kutumia mita zilizonunuliwa hivi maajuzi.
Kulingana naye, maombi ambayo hayajashughulikiwa kufikia sasa ni 236,924 na chini ya mpango wa majibu ya haraka ulioanzishwa wiki hii, mita 10,759 zimewekewa wateja wapya.
Siror alisema wateja wengi wamelazimika kusubiri kwa muda kupata stima kwa sababu ya kesi zilizokuwa zikiendelea mahakamani zilizozuia manunuzi ya mita na vifaa vingine.