Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ameihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa Kenya ni salama licha ya ghasia kushuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, alisema hayo alipowasiliana na balozi za mataifa ya kigeni jana Jumanne.
Kulingana na Mudavadi, maandamano yaliyoitishwa na vijana wa kizazi cha Gen Z kupinga mswada huo yalianza kwa amani lakini sasa yamekumbwa na ghasia na uporaji.
“Wiki iliyopita, hali ilibadilika na kuwa tisho kwa usalama wa taifa huku mashambulizi yakilenga majengo ya bunge, Idara ya Mahakama na afisi ya Gavana wa Nairobi. Mashambulizi yaliyopangwa dhidi ya taasisi zinazowakilisha demokrasia na sheria, yalikuwa bayana,” alisema Mudavadi.
Hata hivyo, Mudavadi aliwaambia mabalozi hao kuwa serikali itakabiliana vilivyo na makundi ya wahalifu huku ikidumisha usalama na amani kote nchini.
“Nawahakikishia kwamba usalama wa Kenya hautahujumiwa na kwamba serikali imechukua mikakati kabambe ya kukabiliana na maandamano ambayo yanageuka kuwa ghasia.”
Alisema serikali imepokea malalamishi yaliyoibuliwa na vijana, hasaa kuhusu maswala ya ukosefu wa ajira, gharama ya juu ya maisha, kutengwa kisiasa na fursa finyu za kutekeleza uwezo wao wa uvumbuzi.
Mudavadi aliongeza kuwa serikali imejikuta pagumu katika kuamua iwapo italipa madeni ya taifa hili au ishughulikie hisia za wananchi.
Aliwahakikishia mabalozi hao kuwa Rais William Ruto yuko tayari kushiriki meza ya mazungumzo na vijana, kujadili mustakabali wa taifa hili kuhusu changamoto za uongozi, mzigo wa madeni, misukosuko ya kiuchumi na kisiasa.
Pia alisisitiza umuhimu wa majadiliano ya pamoja kusuluhisha hisia hizo.