Naibu Rais Kithure Kindiki amesema nchi iko salama chini ya serikali ya Kenya Kwanza.
Akizungumza na wanahabari katika jumba la Harambee Annex jijini Nairobi, Kindiki ambaye alitoa hotuba yake ya kuondoka kama waziri wa hivi punde wa usalama wa taifa, alisema mageuzi katika idara za usalama wa taifa yaliyoanza Disemba mwaka 2022 yanazaa matunda.
Kulingana na Kindiki taifa hili sasa linanakili visa vichache vya wizi wa mifugo, ugaidi na visa vya uhalifu mwingine.
Alisema chini ya uongozi wake, maeneo ya Lamu na Kaskazini Mashariki sasa yako salama na tulivu, huku vita dhidi ya ujangili katika aneo la North Rift vikizaa matunda.
Kindiki pia alisifia mradi wa uimarishaji wa kisasa, wa vifaa vya polisi ulioanzishwa mwaka wa 2023, akisema ulikuwa umeboresha utoaji huduma kisasa katika kukabiliana na uhalifu.
Alisema alifanikiwa kuondoa mrundiko wa uchakataji wa pasipoti, na kupunguza muda wa kusubiri kutoka miezi 12 hadi siku saba sasa.
Kindiki alitoa wito kwa zaidi ya watu elfu 85 waliotuma maombi kuchukua pasipoti zao.
Alisema wahusika wa ufisadi katika ofisi ya uahamiaji walikuwa wamechukuliwa hatua, huku viongozi wakuu 17 wakipitia mkondo wa sheria kwa sasa.
Kindiki aliwashukuru maafisa wote kwa kujitolea kwao katika utoaji huduma, na kutoa changamoto kwa mridhi wake kushughulikia visa vya utekaji nyara na kutoweka kwa watu, na pia mauaji ya watu wa jinsia ya kike ambavyo vinaongezeka nchini.