Kenya ni kitovu cha amani na uthabiti, asema Mudavadi

Tom Mathinji
1 Min Read

Waziri mwenye mamlaka makuu ambaye pia waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi, amekariri kujitolea kwa serikali kuhakikisha amani na uthabiti vinadumishwa hapa nchini.

Mudavadi amesema Kenya ni kielelezo cha amani na uthabiti sio tu katika kanda hii, lakini barani Afrika, huku akiwahimiza Wakenya kuendelea kudumisha amani kwa ajili ya ustawi wa taifa hili.

Akiongea alipofungua mkutano wa chama cha kimataifa cha Sri Sathya Sai mjini Nairobi, Mudavadi alisema utawala wa kidemokrasia na kisheria umeinua hadhi ya taifa hili katika jamii ya kimataifa.

“Tunapaswa kukabiliana na changamoto kupitia kuhimizana na mazungumzo,” alisema Mudavadi.

Alielezea umuhimu wa kutatua mizozo kwa njia ya amani, na majadiliano kuhusu maswala yanayoathiri maisha ya kila siku ya watu.

“Katiba yetu inaelezea kuhusu uhuru wa kujieleza, inasisitiza kuhusu majadiliano bila ghasia kutatua mizozo,” aliongeza Mudavadi.

Mudavadi kadhalika alipongeza chama cha Sri Sathya Sai kwa kujihusisha katika shughuli zinazobadili maisha ya watu, akitoa mfano wa kampeni yake ya matibabu ya hivi majuzi katika nchi za Kenya,Uganda na Tanzania.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *