Kenya na UAE zasaini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo iliongozwa na Rais William Ruto na Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais wa UAE katika mji wa Abu Dhabi.

Marion Bosire
3 Min Read

Katika hatua ya kihistoria, Kenya na Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE) leo zimetia saini mkataba wa ushirikiano wa kina wa kiuchumi, hatua muhimu katika uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili.

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo iliongozwa na Rais William Ruto na Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, Rais wa UAE katika mji wa Abu Dhabi.

Mkataba huo ni wa kwanza kufikiwa kati ya UAE na nchi ya bara Afrika na unaashiria hatua ya mageuzi katika kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Unalenga kukuza nafasi ya Kenya kama lango kuu la Afrika Mashariki na Kusini, huku ukimarisha nafasi ya UAE kama kituo cha kimataifa cha usafirishaji na fedha kinachounganisha Mashariki ya Kati, Asia na maeneo mengine duniani.

Biashara kati ya nchi hizi mbili imeongezeka kwa kasi katika muda wa miaka kumi iliyopita, ambapo biashara jumla ya mwaka 2023 ilifikia shilingi bilioni 445.

UAE ni nchi ya sita kwa ukubwa kama soko la bidhaa za Kenya na ni chanzo cha pili kikubwa cha bidhaa za kuagiza.

Bidhaa kuu zinazouzwa kutoka Kenya ni pamoja na mazao ya kilimo kama vile nyama, mboga, matunda na maua, huku UAE ikitoa bidhaa muhimu kwa Kenya kama mafuta ya petroli na mashine.

Makubaliano yaliyoafikiwa yanalenga kuimarisha uhusiano wa biashara kwa kuondoa vikwazo vya biashara, kurahisisha taratibu za forodha na kukuza viwanda na mifumo ya thamani katika kanda.

Kando na biashara ya bidhaa, mkataba huo unajumuisha huduma, biashara ya kidijitali na ubunifu wa kiteknolojia, na kutoa fursa mpya kwa watoa huduma wa Kenya katika sekta kama elimu, usafiri na ujenzi.

Unawiana na Mpango wa Mageuzi ya Kiuchumi wa Kenya wa Bottom-Up (BETA) na unatarajiwa kufungua masoko mapya, kuvutia wawekezaji wa moja kwa moja kutoka nje na kukuza uhamishaji wa teknolojia.

Nchi zote mbili pia zimejizatiti katika kukuza uendelevu kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi wa kijani na teknolojia safi.

Mkataba huu unaunga mkono mkakati mpana wa biashara wa Kenya, ambao unajumuisha ushirikiano muhimu na Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani.

Kwa khakikisha upatikanaji wa soko la kimataifa bila vikwazo vya kodi, Kenya inaendelea kujitokeza kama taifa muhimu katika uchumi wa kimataifa.

Mkataba huo wa Kenya na UAE unatarajiwa kuleta mageuzi ya kiuchumi, ukitoa fursa mpya katika sekta kama nishati, kilimo, afya, na teknolojia ya mawasiliano, huku ukiimarisha zaidi uhusiano kati ya mataifa haya mawili.

Rais Ruto aliondoka nchini jana kuelekea UAE kuhudhuria kongamano la Abu Dhabi kuhusu uendelevu yaani ADSW.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *