Kenya na Tanzania kusuluhisha mzozo wa safari za ndege

Tom Mathinji
2 Min Read

Saa chache baada ya Serikali ya Tanzania kupiga marufuku safari za ndege za abiria za shirika la Kenya Airways KQ, Kati ya Nairobi na Dar es Salaam, nchi hizo mbili sasa zimeafikia kutatua mzozo huo.

Waziri mwenye mamlaka Makuu Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa mambo ya nje, alisema amefanya mazungumzo na mwenzake wa mambo ya nje wa Tanzania January Makamba kuwa mataifa hayo mawili yako tayari kusuluhisha mzozo huo.

Kupitia mtandao wake wa X, Mudavadi alisema,” Nimezungumza na Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, na tumekubaliana kwamba halmashauri za kusimamia safari za ndege za nchi hizi mbili  zifanye kazi kwa pamoja ili kusuluhisha swala hilo,”.

Aidha kwa upande wake Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania January Makamba kupitia mtandao wa X, alisema mamlaka katika nchi zote mbili zimejitolea kutatua suala hilo kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo.

Naye Waziri wa barabara na uchukuzi wa Kenya Kipchumba Murkomen, alisema ameanzisha mazungumzo na mwenzake wa Tanzania profesa Makame Mbarawa, kwa lengo la kuhakikisha marufuku hayo yanaondolewa.

Siku ya Jumatatu Mamlaka ya Usafiri wa anga nchini Tanzania, ilitangaza kusitisha safari za ndege za abiria za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) kuanzia Januari 22, mwaka huu.

Hatua hiyo ilitokana baada ya Mamlaka ya Ndege nchini Kenya kukataa ombi la Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuruhusu ndege ya mizigo ya Air Tanzania kusafirisha mizigo kutoka Nairobi kwenda mataifa mengine.

Website |  + posts
Share This Article