Rais William Ruto siku ya Jumatatu akiwa Atlanta, Georgia, alishuhudia kutiwa saini kwa mikataba ya maelewano inayolenga kupiga jeki sekta ya afya nchini Kenya.
Mikataba hiyo ya maelewano ilikuwa kati ya kituo cha Marekani cha kudhibiti magonjwa CDC, taasisi ya utafiti wa matibabu nchini KEMRI, wizara ya afya na mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi nchini Kenya.
Wakati wa ziara yake katika makao makuu ya kituo cha kukabiliana na magonjwa Atlanta, Rais Ruto aliyeandamana na waziri wa afya Susan Nakhumicha, alielezea kuimarisha ushirikiano wa sekta za afya za Kenya na Marekani, kwa lengo la kupanua viwanda vya utenegenezaji dawa hapa nchini.
Kiongozi huyo wa taifa, alipongeza serikali ya Marekani kwa kuwa mshirika wake muhimu kwa maendeleo ya sekta ya afya hapa nchini.
“Marekani imekuwa mshirika muhimu wa Kenya katika sekta ya afya, kuanzia miundomsingi na utafiti wa magonjwa ya kuambukiza. Tunalenga kuimarisha ushirikiano huu, ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa dawa humu nchini kwa manufaa ya wote,” alisema Rais Ruto.
Kituo cha kudhibiti magonjwa cha Marekani CDC, kimeisaidia Kenya pamoja na washirika wa kimataifa kuimarisha juhudi za kukabiliana na Ukimwi na kifua kikuu, kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na UKIMWI.