Kenya na Marekani zatia saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya elimu

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais William Ruto amesema serikali imeimarisha zaidi uhusiano wa muda mrefu kati ya Kenya na Amerika kwa kutia saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya elimu.

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini kati ya vyuo vikuu vya Kenya na vile vya Marekani, yanalenga kuimarisha uwezo wa kidijitali.

Kulingana na Rais Ruto,makubaliano hayo yatawezesha wanafunzi zaidi kutoka Kenya kuendeleza masomo yao nchini Amerika, pamoja na kuwezesha utafiti wa pamoja baina ya taasisi za elimu kwenya mataifa haya mawili.

Rais Ruto alikariri kwamba taasisi za elimu ya juu nchini Kenya zitaendelea kushirikiana na zile za Amerika katika uzinduzi wa mikakati ya kuwezesha wanafunzi kupata elimu inayostahili na ujuzi unaohitajika katika sekta mbali mbali za kiuchumi.

“Ninapendekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya wataalam wa Amerika, vyuo vikuu, vyuo anuwai na taasisi za kiufundi za Kenya,” alisema Rais Ruto.

Aidha Rais ruto alisikitikia idadi ndogo ya wanawake katika Sayansi, Teknolojia, uhandisi na Hisabati (STEM), akidokeza hali hiyo inatoa changamoto ya maendeleo katika sekta zingine.

“Licha ya ushahidi uliopo kuhusu hatua zilizopigwa, Kenya inakumbwa na changamoto ya kuwepo kwa pengo katika STEM kuanzia kwa elimu hadi kwa ajira. Ushirikiano wetu unapaswa kulenga kuimarisha ushiriki wa wanawake katika STEM,” alidokeza Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa alisema hayo siku ya Jumanne katika chuo cha Spelman Atlanta, Georgia, nchini Amerika.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article