Serikali za Kenya na Marekani zitaandaa kongamano kubwa la uchumi wa ubinifu baadaye mwaka huu.Haya yaliafikiwa katika mkutano kati ya waziri wa masuala ya vijana, uchumi wa ubunifu na michezo Salim Mvurya na balozi wa Marekani nchini Kenya Marc Dillard.
Kongamano hilo linalolenga kuimarisha ubinifu na ustawishaji wa talanta linatizamiwa kuwakutanisha wabunifu kutoka nchi hizo mbili ambao watabadilishana mawazo na kuongeza fursa za sekta ya ubunifu ikiwemo tasnia ya filamu.
Waziri Salim Mvurya, ameelezea kwamba mpango huu ulitokana na mazungumzo yaliyofanyika wakati wa ziara ya Rais William Ruto huko Atlanta nchini Marekani mwaka jana.
Alisisitiza kuhusu kujitolea kwa Kenya kuimarisha sekta ya uchumi wa ubunifu ambayo imekuwa chanzo muhimu cha mapato kwa vijana kote nchini.
“Tunaangazia kuwezesha wabunifu kiuchumi na kutoa fursa za ukuaji. Tunatizamia michango yenye athari kutoka kwa wabunifu wa Marekanikatika kongamano hilo.” alisema Mvurya.
Balozi wa Marekani nchini Kenya Marc Billard, alitoa maoni sawia huku akithibitisha kujitolea kwa Marekani kusaidia katika maendeleo ya vijana na ushirikiano kati ya tamaduni tofauti.
“Vijana ndio mustakabali wetu na kuwaundia fursa zinazounganisha talanta, ujuzi na maarifa kati ya Kenya na Marekani kunasalia kuwa lengo letu kuu.” alisema balozi Billard.
Waziri Mvurya aliendelea kusema kwamba serikali ya Kenya inaharakisha sera na mifumo ya kisheria ili kukuza mazingira ya kulea vipaji vya ubunifu vya vijana na kuwahimiza kubuni na kufuata ndoto zao.
Kongamano hilo linatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha maisha ya vijana wabunifu na kuendesha ukuaji wa muda mrefu wa sekta ya ubunifu nchini Kenya.