Kenya na Korea Kusini kuunda kamati ya pamoja ya kiuchumi

Martin Mwanje
1 Min Read

Kenya na Korea Kusini zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja ya kiuchumi.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na biashara kati ya nchi hizo mbili.

Marais William Ruto wa Kenya na Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini walikubaliana kuunda kamati hiyo walipozungumza kwa njia ya simu leo Alhamisi pembezoni mwa mkutano unaoendelea wa siku mbili unaoangazia utendakazi wa seriikali ya Kenya katika mtaa wa South C, Nairobi.

Kamati hiyo inatarajiwa kuharakisha nyanja za ushirikiano zilizokubaliwa wakati wa ziara ya Rais Ruto nchini Korea Kusini mwaka jana.

Nyanja hizo ni Jiji la Kidijitali la Konza, Mradi Pevu wa Uchukuzi wa Nairobi na mpango wa ujenzi wa uwezo katika uzalishaji wa chanjo jijini Nairobi.

Kenya na Korea Kusini ni nchi thabiti za kidemokrasia zinazofanya chaguzi zenye ushindani mara kwa mara.

Kwa misingi hiyo, nchi hizo mbili zitaandaa Kongamano la Tatu la Demokrasia kwa ajili ya Siku Zijazo jijini Nairobi mwezi Machi mwakani.

Viongozi hao wawili aidha walizungumzia Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Korea Kusini na Afrika utakaofanywa mwezi Juni mwakani.

Rais Ruto amethibitisha kuwa atahudhuria mkutano huo.

 

Share This Article