Kenya na Japani zimetia saini mkataba wa ushirikiano wa sekta za umma na kibinafsi katika sekta ya uchukuzi.
Utiaji saini huo ulifanywa kati ya Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa Kenya Kipchumba Murkomen na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japani Kokuba Konosuke pembezoni mwa kongamano la pili la miundombinu bora kati ya nchi hizo mbili lililofanyika jijini Nairobi.
“Mkataba huo wa ushirikiano utaanzisha mipangilio mahususi ya kikazi kati ya nchi hizi mbili ambayo itawezesha mawasiliano mazuri na njia ya kufanya kazi ili kuhakikisha ushirikiano utakikanao katika kuhamasisha na kuongeza miradi ya ushirikiano kati ya sekta ya umma na kibinafsi nchini Kenya,” alisema Waziri Murkomen wakati wa kuidhinisha mkataba huo.
“Wizara yangu inapongeza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Kenya na Japani kama mshirika wa maendeleo na rafiki.”
Kenya imeshirikiana na Japani katika kutekeleza miradi mbalimbali katika kipindi cha miaka 60 ya uhusiano.
Miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa barabara ya Ngong jijini Naiorbi na ujenzi wa madaraja katika kaunti za Mombasa na Kilifi.
Kadhalika, Japani pia inahusika katika utekelezaji wa miradi mipya mikubwa kama vile ujenzi wa daraja la Mombasa Gateway ambalo litakuwa refu barani Afrika.
Daraja hilo linatarajiwa kurahisisha usafiri wa watu na usafirishaji wa bidhaa kati ya kisiwa hicho na Pwani Kusini na vile vile kuvutia utalii.
Waziri Murkomen aliisifia miradi ya miundombinu ya ubora wa juu ya Japani akisema inakidhi viwango vilivyowekwa na katiba ya Kenya.