Kenya na Japani zaandaa kongamano la miundombinu bora

Martin Mwanje
1 Min Read

Kenya na Japani zimeandaa kongamano la pili la miundombinu bora baina ya nchi hizo mbili. 

Kongamano hilo liliandaliwa katika hoteli moja jijini Nairobi na kuhudhuriwa na Waziri wa Barabara na Uchukuzi wa Kenya Kipchumba Murkomen na Naibu Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Uchukuzi na Utalii wa Japani Kobuka Konosuke.

Balozi wa Japani nchini Kenya Okaniwa Ken na Mwakilishi Mkuu wa Shirika la Japani la Ushirikiano wa Kimataifa, JICA Shinkawa Makoto ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu waliohudhuria kongamano hilo.

“Kongamano hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za umma na kibinafsi katika mataifa ya Kenya na Japani, na kutafuta fursa mpya za miundombinu, hasa kwa kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi,” amesema Waziri Murkomen ambaye baadaye alifanya mazungumzo na Konosuke.

Mazungumzo kati yao yaliangazia miradi ya maendeleo inayofanyiwa kazi na nchi hizo ikiwa ni pamoja na Mradi wa Maendeleo wa Barabara za Eneo la Bandari ya Mombasa, MPARD na Daraja la Mombasa Gateway.

Kenya na Japani zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia na mwaka uliopita, ziliadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwa uhusiano huo.

Share This Article