Kenya na Italia zimeazimia kuendeleza mazungumzo kuhusu mkataba wa maelewano kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya.
Wakati wa mkutano, katibu katika wizara ya afya Mary Muthoni Muriuki na naibu balozi wa Italia Lorenza Gambacorta, waliimarisha mazungumzo kuhusu mkataba wa maelewano unaolenga kuboresha utoaji wa huduma nafuu za afya kwa wote na utengenezaji wa dawa.
Mkutano huo unafuatia ule wa awali ambapo Rais William Ruto na mwenzake wa Italia Sergio Mattarella, walitia saini mkataba wa maelewano, wakati wa ziara ya Rais Mattarella hapa nchini mwezi Machi mwaka 2023.
Ziara hiyo ilisababisha kutiwa saini kwa mikataba ya maelewano iliyojumuisha, ubadilishanaji wa maarifa ili kuimarisha mifumo ya afya, utengenezaji wa dawa hapa nchini, taasisi za utafiti za humu nchini na zile za Italia kushirikiana katika utafiti, utoaji mafunzo na huduma za afya miongoni mwa mingine.
Kulingana na katibu huyo, ushirikiano huo baina ya Kenya na Italia ni muhimu sana katika kuboresha utoaji wa huduma nafuu za afya kwa wote.