Kenya imeanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia na taifa la Haiti.
Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry walishuhudia kutiwa saini kwa mkataba wa maelewano katika afisi ya ubalozi ya Kenya jijini New York, Marekani.
Mkataba huo uliotiwa saini na Mawaziri Jean Victor Génus wa Haiti na Alfred Mutua wa Kenya unatoa mwelekeo kuhusu ushirikiano katika nyanja mbalimbali za manufaa kwa mataifa haya mawili.
Rais Ruto alitoa wito wa ushirikiano kamili katika nyanja kama vile siasa, usalama na hata maendeleo ili kushughulikia hali inayojiri nchini Haiti.
Kulingana naye, Kenya itatekeleza jukumu lake katika kuongoza ujumbe wa kiusalama ulio na vifaa hitajika na wenye ufanisi kutoka nchi mbalimbali nchini Haiti.
“Kama nchi inayoongoza mpango wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Haiti, tumejitolea kutuma kikosi maalumu kuchunguza hali ilivyo nchini humo na kuandaa mikakati inayoweza kutekelezwa na ambayo itatoa suluhisho la kudumu,” alisema Rais.
Waziri Mkuu Henry kwa upande wake alisema Haiti inahitaji usaidizi kutatua changamoto zilizokithiri katika sekta za usalama, mahitaji ya kibinadamu, mazingira na uchumi.
Kulingana naye, watu wa Haiti wanatizamia kwa matumaini makubwa kuondolewa kabisa kwa makundi yaliyojihami ambayo yamekuwa yakitekeleza mashambulizi nchini humo tangu mwaka 2021.