Kenya na EU zaungana kupambana na ukeketaji

Martin Mwanje
2 Min Read

Mji wa Iten katika kaunti ya Elgeyo Marakwet leo Ijumaa ulikuwa kitovu cha mkutano uliowaleta pamoja Gavana Wisley Rotich, Balozi wa Umoja wa Ulaya, EU nchini Kenya Henriette Geiger, na Sadia Hussein ambaye ni mwasisi wa shirika la Brighter Society Initiative miongoni mwa viongozi wengine.

Huku ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, viongozi hao walikutana chini ya kaulimbiu “Elimu Siyo Ukeketaji.”

Mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Iten ulikuwa hatua kubwa kuelekea utokomezaji wa ukeketaji humu nchini, hususan katika kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Kaunti hiyo imekumbwa na visa vingi vya ukeketaji.

Kwa kurejelea maudhui ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu ambayo ni “Hamasisha Ujumuishaji”, mkutano huo uliangazia uwezo wa elimu na utamaduni dhidi ya itikadi kandamizi.  

Balozi Geiger alisisitiza umuhimu wa ujumuishaji na uwezo wa elimu katika kupigana na ukeketaji.

“Wakati tunapowahamasisha wengine kuelewa na kuthamini ujumuishaji wa wanawake, tunatengeneza dunia bora. Elimu ni mnara wa matumaini. Inaangazia hatari za ukeketaji, ikionyesha kuwa itikadi hii haina faida ya kiafya, ila madhara tu,” alisema Balozi Geiger.

“Uwepo wetu Iten Iten hii leo unasisitiza dhamira yetu isiyoyumba ya kuangamiza ukeketaji na kusherehekea urathi wa utamaduni wenye utajiri wa Elgeyo Marakwet wakati tukipigania haki na afya ya wanawake na wasichana.”

Kwa upande wake, Hussein ambaye amekuwa mnara wa mabadiliko katika jamii hiyo alisema, “Kama mwathiriwa wa ukeketaji, singependa msichana yeyote kupitia yale yaliyonikumba. Wasichana wanastahili kupata elimu, siyo kukeketwa”.

Share This Article