Kenya imetia saini mkataba maalum wa pamoja wa ushirikiano na Colombia jijini Bogota, katika juhudi za kuboresha uhusiano baina ya mataifa haya mawili.
Kutiwa saini kwa mkataba huo wa ushirikiano kunatoa fursa mpya ya kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, jinsia, elimu, sayansi na teknolojia, ubadilishanaji wa utamaduni, uchukuzi, Afya, uhifadhi wa mazingira, biashara na uwekezaji, miongoni mwa maswala mengine.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, naibu rais Rigathi Gachagua alisema kuwa mazungumzo kuhusu njia za kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili kupitia safari za ndege za moja kwa moja yanakaribia kukamilika.
Hatua hii inalenga kuimarisha utangamano na usafirishaji wa bidhaa na huduma.
Naibu rais alisema Kenya ilifanya majadiliano juu namna ya kusitisha mahitaji ya visa kwa wenye pasipoti za kidiplomasia na pasipoti za huduma.
Alidhibitisha kujitolea kwa serikali ya Kenya kushirikiana na Colombia kuhakikisha kutekelezwa kikamilifu kwa yaliyoafikiwa.
Kutiwa saini kwa mkataba huo kuliongozwa na waziri wa mambo ya nje wa Kenya Dkt. Alfred Mutua, makamu wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Colombia Francisco Coy.