Kenya inalenga kuimarisha ushirikiano wake na China hasa katika ubadilishanaji wa habari za ujasusi, operesheni za pamoja za kiusalama na usimamizi wa maswala ya usalama.
Katibu katikaUwizara ya Usalama wa Taifa Dkt. Raymond Omollo, amesema hatua hiyo itatekeleza jukumu muhimu kwa taifa hili kukabiliana na vitisho vya usalama.
Omollo alitaja ugaidi, uhalifu wa mtandaoni, mizozo ya kanda na mabadiliko ya tabia nchi, kuwa tisho la amani duniani.
Aliyasema hayo siku ya Jumanne katika mkutano wa ushirikiano wa kiusalama ulioandaliwa Lianyungang nchini China.
Omollo alidokeza kuwa mkutano huo unaweka jukwaa kwa Kenya na China kushiriki mazungumzo na kuweka mikakati inayounganisha nchi hizi mbili katika kutafuta amani, usalama na ushirikiano wa maendeleo.
Aidha, alisema kuwa Kenya inalenga kushirikiana zaidi katika mikataba ya usalama na China na washirika wengine.
Alisema maafisa wa polisi wa Kenya wamekuwa wakipata mafunzo ya kiufundi kuhusu usalama kutoka China, huku akiongeza kuwa mafunzo hayo yanapaswa kupanuliwa zaidi ili kujumuisha asasi zingine za usalama.