Kenya Kwanza yataja timu itakayoshiriki mazungumzo na Azimio

Martin Mwanje
2 Min Read

Utawala wa Kenya Kwanza umetaja timu ya watu watano watakaoshiriki mazuungumzo na muungano wa upinzani wa Azimio. 

Timu hiyo itakayoongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah inajumuisha Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, Gavana wa Embu Cecily Mbarire, Mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Bungoma Catherine Wambilianga na mbunge wa EALA Hassan Omar.

Katika taarifa, Kenya Kwanza imesema tiimu yake imejukumiwa kushiriki mazungumzo yatakayoangazia hoja tano, nazo ni uundaji upya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, utekelezaji wa sheria ya jinsia na Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge, CDF.

Hoja zingine ni kubuniwa kwa ofisi ya kiongozi wa upinzani na uangaziaji wa Ofisi ya Waziri Mwenye Mamlaka Makuu.

“Ili kuondoa dukuduku, kama ilivyokubaliwa, vurugu kamwe haitakuwa na daima haitakuwa sehemu ya mazungumzo ya kitaifa ya kisiasa na hakutakuwa na mazungumzo ya namna yoyote kuhusiana na masuala ya serikali ya muungano au nusu mkate,” ilisema taarifa ya Kenya Kwanza.

Upande wa Azimio umetaja timu ya watu watano itakayoongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka. Wanachama wengine ni kiongozi wa wachache katika bunge la taifa Opiyo Wandayi, Seneta Okong’o Omogeni, mbunge wa Malindi Amina Mnyanzi na Waziri wa zamani wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

Kwa kuzingatia taarifa ya timu hiyo, hali ya vuta ni kuvute inajadiliwa kushuhudiwa kati ya pande hizo, kwani upande wa Azimio umeapa kuwa suala la gharama ya maisha ni lazima liwe sehemu ya mazungumzo hayo.

Hata hivyo, Kenya Kwanza inasema imeweka mikakati kabambe ya kushughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja na kushusha bei ya mbolea ya bei nafuu hadi shilingi 2,500 na kwa misingi hiyo, mazungumzo hayatasaidia kwa namna yoyote kuangazia suala hilo.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *