Kenya Kwanza yaisihi Azimio kujerea kwenye meza ya mazungumzo

Martin Mwanje
1 Min Read

Muungano wa Azimio umetakiwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kati ya upinzani na serikali ya Kenya Kwanza. 

Muungano huo ulijiondoa kwenye mazungumzo ya pande mbili na utawala wa Kenya Kwanza ikitaja kushindwa kwa serikali kuangazia masuala ulioibua ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa mswada wa fedha wa mwaka 2023 na gharama ya juu ya maisha.

Azimio badala yake iliitisha maandamano ili kuishinikiza serikali kuangazia masuala hayo, hatua ambayo imeonekana kutoambulia chochote.

Muungano huo ulitangaza kusitishwa kwa maandamano yaliyoratibiwa kufanyika kesho Jumatano baada ya maandamano ya awali kukumbwa na vurugu zilizosababisha vifo vya watu kadhaa na wengine kujeruhiwa.

“Tunaushukuru muungano wa Azimio kwa kusitisha maandamano,” alisema George Murugara, mwenyekiti mwenza wa kamati ya bunge inayosimamia mazungumzo kati ya Kenya Kwanza na Azimio.

“Kwa mara nyingine, tunatoa wito kwa Azimio waje tushiriki meza ya mazungumzo,” alisema Murugara wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumanne.

Alipoulizwa ikiwa kamati hiyo inaweza ikawakubalia washikadau mbalimbali kushiriki mazungumzo hayo ikiwa yatarejelewa, Murugara alisema hiyo haiwezekani kwa sababu hiyo ni kamati ya bunge.

Hata hivyo, alisema ikiwa wadau wengine wana maoni kuhusu mazungumzo hayo, wako radhi kuyawasilisha kwa kamati hiyo ili yazingatiwe.

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *