Suala la kupanda kwa gharama ya maisha ni miongoni mwa masuala matano makuu yatakayojadiliwa na kamati ya mazungumzo ya pande mbili.
Suala hilo lilikuwa tata huku mrengo wa Kenya Kwanza ukishikia kuwa serikali tayari inatekeleza mipango kabambe ya kupunguza gharama ya maisha ikiwa ni pamooja na kupitia utoaji mbolea ya bei nafuu ili kuongeza uzalishaji wa chakula.
Kwa upande mwingine, upande wa Azimio ulitishia kurejelea maandamano ikiwa suala hilo lingepewa kisogo ukidai mzigo wa gharama ya maisha umewaelemea Wakenya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumatano na Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo, NADCO chini ya uenyekiti wenza wa kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah, uchaguzi wa urais wa mwaka 2022 pia utafanyiwa ukaguzi.
Mrengo wa Azimio umekuwa ukidai ulishinda uchaguzi huo, madai ambayo utawala wa Kenya Kwanza umeyapuuzilia mbali ukisema hata Mahakama ya Juu ilibaini kuwa ulishinda uchaguzi huo.
Kimsingi, masuala matano makuu yatakayojadiliwa na kamati ya mazungumzo baada ya kuidhinishwa na kamati hiyo ni masuala ya kikatiba ambayo bado hayashughulikiwa, haki katika uchaguzi na masuala husika, ujumuishaji wa hazina ikiwa ni pamoja na hazina ya serikali ya kitaifa ya maendeleo katika maeneo bunge na ile ya kitendo sawazishi kwenye katiba, uanzishaji na uwekaji kwenye sheria ofisi za kitaifa ikiwemo ile ya kiongozi wa upinzani na waziri mwenye mamlaka makuu na kuheshimu vyama na miungano ya kisiasa na sheria kuhusu demokrasia ya vyama vingi.
Uundaji mpya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC na utengenezaji mipaka ni masuala ambayo pia yatamulikwa na kamati ya mazungumzo.