Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amesema Kenya iko tayari kushirikiana na kampuni kutoka Korea Kusini katika sekta za utengenezaji bidhaa, teknolojia ya viwandani, nishati mbadala, ujenzi, uhandisi na maendeleo ya miji ya kisasa.
Mudavadi alidokeza kuwa Kenya inajitahidi kuimarisha mazingira mwafaka ya uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati na kampuni za Korea Kusini.
“Kenya ni kiingilio cha soko la watu zaidi ya milioni 500 katika kanda ya Afrika Mashariki, ikipigwa jeki na demokrasia thabiti, nguvukazi iliyoimarika na miundombinu ya kisasa,” alisema Mudavadi.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alisema kuwa Korea Kusini imekuwa mfano bora duniani katika ufanisi wa kiviwanda, na Kenya inalenga kushirikiana na taifa hilo kwa mustakabal thabiti uliojikita kwenye uvumbuzi, maarifa na ufanisi wa pamoja.
“Kenya haiko tayari tu kwa biashara, tunalenga ushirikiano utakaobuni nafasi za ajira, ubadilishanaji wa maarifa na kuanzishwa kwa viwanda vitakavyobainisha mustakabal wetu. Tunathamini sana kampuni za Korea Kusini kwa ubora wao wa hali ya juu, uvumbuzi na kujitolea kwa muda mrefu,” aliongeza Mudavadi.
Waziri huyo aliyasema hayo alipokutana na wawakilishi wa viwanda vya Korea Kusini pamoja na wale wa mashirika ya kijamii alipozuru Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknoloji acha Gyeonggi (GTEC) katika jiji la Siheung, mkoa wa Gyeonggi.