Wizara ya afya imejizatiti kuimarisha hatua za kukabili matumizi ya bidhaa za tumbako hapa nchini kwa ajili ya kuboresha afya ya wananchi.
Katibu wa afya ya umma Mary Muthoni alisema watazindua mikakati maksusi ya kukabili ukiukaji wa sheria za kudhibiti matumizi ya tumbako hapa nchini.
Akikiri kuwa taifa hili linakumbwa na changamoto za udhibiti wa bidhaa za tumbako nchini, pamoja na kudumisha sheria za kukabili matumizi ya bidhaa hizo, katibu huyo siku ya Jumatatu alifanya mkutano na wadau tofauti kwa ajili ya kuimarisha vita dhidi ya matumizi ya bidhaa hizo.
“Sheria hizi za kimataifa, zimejumuishwa katika sheria za humu nchini za uthibiti wa tumbaku na hivyo kusababisha kuanzishwa kwa vita dhidi ya matumizi ya tumbako. Kenya imejitolea kuwalinda wananchi wake dhidi ya changamoto za kiafya zinazosababishwa na utumizi wa tumbako,” alisema katibu Mary Muthoni.
Alisisitiza kwamba juhudi hizo za pamoja zitachangia pakubwa harakati za taifa hili za kuthibiti matumizi ya bidhaa za tumbako kwa ajili ya afya ya wananchi.
Taifa hili limeshuhudia visa kadha vya ukiukaji wa sheria za kudhibiti sekta hiyo huku wabunge wakiitaka wizara ya afya kupiga marufuku baadhi ya bidha za tumbako nchini.
Wizara hiyo iliahidi kubuni kamati ya wataalam kuchunguza upya sheria za kuthibiti sekta hiyo na kuwasilisha mapendekezo yake.