Timu ya taifa ya raga ya Kenya kwa wanaume saba upande maarufu kama Shujaa, itaanza harakati za kuwinda nishani ya Olimpiki katika makala ya 33 Jumatano jioni dhidi ya Argentina kudini B.
Mchuano huo utaanza saa kumina moja jioni, ukifuatwa na ule wa pili dhidi ya Australia saa mbili usiku, na kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Samoa siku ya Alhamisi.
Kenya itakuwa ikishiriki Olimpiki kwa mara ya tatu baada ya kumaliza ya 11, wakishindwa mechi zote mwaka 2016 na pia kuchukua nafasi ya 9 mwaka 2021 mjini Tokyo Japan.
Ili kufuzu kwa Olimpiki ya mwaka huu Shujaa wanaofunzwa na kocha Kevin Wambua, walitwaa ubingwa wa Afrika katika mashindano yaliyoandaliwa nchini Zimbabwe mwaka uliopita.
Timu hiyo inawajumuisha wachezaji 10 wapya huku wawili tu wakiwa Herman Humwa na Vincent Onyala, wakiwa na uzoefu wa kushiriki mashindano ya awali.